Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba ameiagiza Manispaa ya Sumbawanga kuhakikisha wanaandaa mkakati wa kushughulikia tatizo la ongezeko la watoto wa mitaani kwenye mji huo.
Agizo hilo la Mkuu wa wilaya amelitoa wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo ambapo amesema kuwa hali sio shwari kwasababu ya watoto hao kuzidi kuongezeka kwenye baadhi ya mitaa.
Waryuba amesema watoto hao wamekuwa wakionekana sehemu za migahawa na sehemu za vileo wakisubiria kuomba misaada ya fedha na chakula.
“Mimi binafsi huwa nakwenda maeneo ya chakula wakiwa hawajui kuwa ni Mkuu wa wilaya na huwa wananiomba fedha na hata chakula, nawapa lakini pia nawasahili maswali kutaka kufahamu walipo wazazi wao, utasikia baba yuko Ziwa Rukwa, au mama yuko kule, hii inasikitisha” alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Hatahivyo Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga alitaka wadau wengine kushiriki kwenye mpango huo wa kuwaondoa watoto hao mitaani kwani alisema wakiendelea kuachwa ni sawa na bomu linalotengenezwa na likija kulipuka litaathiri watu wengi ndani nan je ya mkoa wa Rukwa.
“Hili Bomu, tukiendelea kulilea litalipuka na likilipuka hapatakalika hapa mjini, hawa watoto hawana malezi na wanaweza wakajiingiza kwenye vitendo vya ujambaza, ukabaji na hata mambo mengine yasiyofaa”alisema Waryuba.
Aidha aliomba Taasisi za Dini na hata watu binafsi kuwasaidia watoto hao waweze kusoma kwani wengi wao wameacha shule na kuanza kuzurura mitaani wakidai kuwa hawana huduma za msingi hivyo kuacha shule.
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa