Wasanii wa fani mbalimbali mjini Sumbawanga, Mkoani Rukwa wameeleza kilio chao juu ya utayarishaji mbovu wa sauti za muziki na picha za video unaofanywa na watayarishaji waliopo ndani ya mkoa na kuwaomba wadau wa sanaa kutoka katika mikoa iliyoendelea katika fani hiyo kuja kuwekeza ili waweze kuleta ushindani katika sanaa.
Kilio hicho kimetolewa baada ya Afisa utamaduni wa Manispaa ya Sumbawanga, Charles Kiheka, kuwaita wasanii hao wa fani mbalimbali ili kujua changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo pamoja kuwaelimisha miongozo na taratibu mbalimbali zinazotakiwa kufuatwa ili kutokiuka taratibu za kiserikali katika kufanya shughuli zao za sanaa.
Mmoja wa wasanii wa Hip-hop, Martin Gondwe amesema kuwa ‘studio’ zilizopo zimekosa vifaa vizuri vitakavyomwezesha msanii aliyerekodi nyimbo yake mjini Sumbawanga kuweza kuleta ushindani katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
“Vile vile tukizungumzia upande wa “video”, wasanii wanakuwa wanafanya nyimbo inakuwa na “quality” (ubora) ndogo, “Audio” inakuwa ya kawaida, pamoja na “video” pia inakuwa ya kawaida yaani kila kitu kibovu, huwezi kuifikisha hiyo nyimbo yako sehemu yoyote,” Alisisitiza.
Nae Steven Stanley, msanii wa Hip-hop aliongeza kuwa kutokana na ubovu wa kazi zinazofanywa na watayarishaji wa muziki katika upande wa sauti na picha inapelekea wasanii wengi kushindwa kuwashawishi wadau wa sanaa na hatimae kukosa kusaidiwa ili kuweza kusonga mbele zaidi.
“”Video” zinakuwa ziko “local” kiasi kwamba huwezi ukamshawishi mtu anunue, kwasababu kila mtu anapenda kitu kizuri, kwahiyo mtu akiona “video” nzuri anasema hii nimeipenda na akiona kitu kibaya anasema piga chini, ila ukosefu wa “production” ndio “una-cost” kabisa, kwasababu siwezi nikarekodi nyimbo hapa ambayo “production” ipo “local” halafu nikatuma Dar,” Alibainisha.
Kwa upande wake Charles Kiheka alileza kuwa wasanii hawatakiwi kusubiri sherehe za kiserikali pekee kama fursa ya kujitangaza bali ni jukumu la msanii kuwa mbunifu katika kuandaa matamasha hayo na hatimae kuonana nae ili kuona namna ya kumsaidia katika kukamilisha mipango ya msanii aliyonayo ili kujiongezea kipato kwa kumpa vibali vyote stahiki pamoja na ushauri wa mikataba mbalimbali anayotaka kuingia na wadau wa burudani.
“Leo hii msanii anakwambia serikali iandae “event” aje “kuperform” wasanii wapo wangapi na matukio ya serikali sio ya kila siku, wewe kama mdau wa sanaa, kama msanii ni jukumu lako kuandaa matukio mbalimbali, unakuja na mipango yako ofisini tunaelekezana namna ya kufanya na kuzitafutia ufumbuzi changamoto unazoweza kukabiliana nazo,”Alisema Kiheka.
Katika juhudi za kuhakikisha wasanii hao wanajifunza namna ya kuandaa matamasha, Kiheka anatarajia kuzindua tamasha la “Amka Kijana, Onesha Kipaji Chako” litakalojumuisha mashindano ya sanaa za fani mbalimbali, kuanzia kuimba, kuigiza, ngoma za asili, pamoja na kucheza nyimbo za kisasa (ku-dance) kabla ya kuisha mwaka 2018.
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa