Na Mwanaidi Waziri
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangambo amewataka wakulima kuachana na kilimo cha mazoea kwa kutumia zana duni za kilimo katika uzalishaji na kujikita katika matumizi ya zana za kisasa ili kuweza kuzalisha mazao mengi zaidi.
Wito huo wa Mkuu wa mkoa umekuja baada ya kutoridhishwa na mavuno yanayopatikana kila mwaka kwa wakulima mkoani Rukwa licha ya kuwa mkoa huo una maeneo mengi yanayofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali.
Alisema hayo katika kikao kilichofanyika ukumbi wa ofisi ya mkoa wa Rukwa kwenye mkutano wa Chama cha Ushirika cha Ufipa Cooperation Union (UCU) kilichofanyika mwanzoni mwa juma kwa lengo la kujadili changamoto mbalimbali za upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima.
Wangabo alisema “ni vyema vyama vya ushirika vihimize matumizi ya zana bora za kilimo kwa wakulima kwenye vyama vyote vya Msingi ili kupanua wigo wa uzalishaji wenye kuleta tija kwa wakulima hao na hata viwanda na uchumi kwa ujumla”
Mkuu huyo wa mkoa alivitaka Vyama hivyo vya Msingi vya wakulima kutumia fursa ya kukopa kutoka kwenye taasisi za kifedha kama vile Benki ya wakulima Tanzania TADB ili kuweza kununua matrekta na hata pembejeo zinginezo.
Naye Meneja wa Kanda Nyanda za Juu Kusini wa benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Dickson Pangamawe alisema vyama vya Ushirika vya wakulima ni daraja kwao la kupata mikopo hiyo ya pembejeo, elimu na zana za kilimo, hivyo kuwataka wakuli a kujiunga pamoja kulingana na maeneo wanakoishi.
“Wakulima wanatakiwa kuacha kutumia jembe la mkono na kujikita katika matumizi ya matrekta ili kulima maeneo makubwa kwa wakati na kupata matokeo ridhishi na kupunguza upotevu mkubwa wa chakula” alisema
Hata hivyo Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika mkoani Rukwa Anyosisye Mbetwa alisema wanataraji kuwasilisha maombi ya mkopo zaidi ya billion 5 kutoka benki ya TADB kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo za kilimo kwenye msimu wa kilimo 2019/20.
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa