Manispaa ya Sumbawanga inatarajia kuongeza mapato yake ya ndani kwa zaidi ya Shilingi Bilioni 1 kila mwaka kutokana na uwekezaji utakaofanywa mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Stendi ya kisasa ya mabasi inayojengwa kwenye eneo la Katumba Azimio nje kidogo ya mji wa Sumbawanga.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Jacob Mtalitinya katika hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa Stendi ya mabasi iliyofanyika Mei 06, 2019 , ikiwa ni moja ya miradi mikubwa kujengwa na Manispaa hiyo.
Mtalitinya alisema mradi huo wa stendi ambao unajengwa na kampuni ya Sumry Enterprises ya mkoani Rukwa unatarajia kugharimu zaidi ya Shilingi Bilioni tano na unatarajiwa kukamilikia mwishoni mwa mwaka huu.
Alisema katika stendi hiyo kunataraji kujengwa sehemu ya maegesho ya mabasi, Daladala, bajaji, bodaboda, Tax zaidi ya 80, vibanda vya kushushia abiria zaidi ya 50, sanjari vyumba vya maduka 300 ambapo kwa kuanzia kutajengwa vyumba 10 kwa kuwa mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa awamu.
Akizungumza kabla kuzindua zoezi hilo la ujenzi Mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo ameipokeza Manispaa ya Sumbawanga hususan Mkurugenzi wake Jacob Mtalitinya kwa ubunifu wa mradi huo ambao utakuwa na fursa kubwa ya kiuchumi na kibiashara kwa wakazi wa Manispaa hiyo.
Mh.Wangabo alisema mradi huo wa stendi ya kisasa unakwenda kufungua eneo jingine la kibiashara katika kijiji cha Katumba na kuzidi kuupanua mji wa Sumbawanga kwani kuna mpango mwingine wa ujenzi wa mji wa kisasa karibu na Stendi hiyo ambapo zaidi ya viwanja 2100 vya makazi, biashara na huduma za kijamii vimepimwa na kuanza kugawiwa wananchi kwaajili ya ujenzi wake.
“Hii Sumbawanga inabadilika, sio Sumbawanga ile ya zamani, nawapongeza sana Manispaa, kwanikupitia stendi hii pia mapato yenu yataongeza kwakuwa katika makadirio ya makusanyo yenu ya mwaka wa fedha 2018/19 mlikadiria kukusanya zaidi ya Bilioni 2.1, sasa hii stendi pekee itawaingiza karibia asilimia 46 ya mapato yenu ya ndani, hongerni sana”.alisema Mkuu huyo wa mkoa.
Kwa upande wao wananchi wa Katumba licha ya kufurahi mradi huo kujengwa kwenye kijiji chao walisema kuwa kijiji chao kimepanda thamani na kuwa mji sasa na kuongeza kuwa tayari wamekwisha ona tija kwenye mradi huo kwani vijana wengi wamepata ajira na akinamama wanafanya biashara ya kuuza bidhaa mbalimba kama vile vyakula.
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa