Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini Aesh Hilaly amewashauri Wataalamu wa ujenzi na wale Elimu katika Manispaa ya Sumbawanga kuanza kufikiria kujenga shule za ghorofa badala ya kujaza nafasi za shule zilizopo majengo kila kona kiasi cha wanafunzi kukosa hata maeneo ya kupumzika.
Ushauri wa Aesh unafuatia ziara ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa madarasa 49 yanayojengwa hivi sasa maaarufu kama madarasa yaUviko-19 ambayo fedha zake zilitolewa na Rais Samia Suluhu ili kukabiliana na upungufu wa madarasa hususan kwenye shule za Sekondari.
Katika majumuisho ya ziara hiyo Aesh alisema kila shule aliyipita ameona hazina mpango kamili wa ujenzi “Lay Out” badala yake kunaonekana maamuzi ya haraka yanayofanywa aidha na Wataalamu au Kamati za Shule au viongozi wa kisiasa ambao pale fedha zinapopatikana na kutakiwa kujengwa madarasa basi huchaguliwa sehemu yoyote kwenye shule husika.
Alisema utaratibu huo umekuwa ukifanyika pasipo kufahamu madhara ya huko mbeleni ambapo shule hizo zinaweza kujikuta hazina maeneo mengine ya kujenga ihali kila kona kumejaa majengo yaliyopishana migongo.
“Huu utaratibu ni mbaya kwani kila mtu akijiamulia hapa pajengwe hivi, kule kuwe vile, mwakani pafanywe hivi, hata sura za shuke zetu hazitaonekana kwasababu utaratibu ni mbovu na zipo baadhi ya shule zimejengwa madarasa kando kuna vyoo na vinatoa harufu kiasi cha kumfanya Mwalimu na Wanafunzi kushindwa kusoma au kufundisha vizuri”.alisema Aesh
Mbunge huyo licha ya kuzitolewa mfano baadhi ya shule za sekondari kama Chanji, Itwelele, alisema suluhu ya haya yote ni ushiriki wa serikali na jamii kutafuta fedha ambazo zitatumika kwaajili ya kujenga misingi imara ya ghorofa mbili au tatu, lakini zinaweza kutumika kujenga sehemu ya chini ambayo yatakuwa madarasa na sehemu ya juu ikaja ikajengwa baadaye kulingana na uwezo wa serikali.
Aesh alisema zipo shule hivi sasa zinajikuta hazina hata maeneo ya kucheza wanafunzi kwasababu kila sehemu kumejazwa majengo huko akitolea mfano shule ya sekondari Mazwi ambayo yeye mwenyewe alisoma kuwa imesongwa na majengo mengi tofauti na zamani ambako kulikuwa na nafasi kubwa ya wazi na wanafunzi wakiitumia kwa michezo mbalimbali.
Alisema pamoja na yote liko pia tatizo kubwa la uhaba wa matundu ya vyoo ambapo kila shule inachangamoto hiyo, hivyo aliwaagiza Wataalamu wa ujenzi kuandaa mchoro ambao utajenga vyoo vya kufanana kwenye shule zote, huku kukiwa na chumba maalumu kwa wanafunzi wa kike kujihifadhi nyakati za hedhi.
Hatahivyo Aesh amemwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya kuandaa eneo maalumu ambalo anatarajia kujenga shule ya mfano ya sekondari ambayo ataisimamia yeye na kisha kuikabidhi halmashauri ili iwe mfano kwa miaka ya sasa na ijayo.
Alisema shule hii italenga hasa kuwapa nafasi watoto wanaosoma shule ya mchepuo wa Kiingereza ya Mwenge B, ikichanganya na wanafunzi wengine kutoka ndani na nje ya mkoa.
“Shule hii nataka iwe bora na ntaijenga kwa kushirikiana na wadau, lakini haitajengwa kwa haraka, nataraji kufanya hivyo ndani ya miaka minne na ikikamilika itaonekana ilivyo, nataka iwe kioo cha mkoa wa Rukwa na watoto watasoma hapo, huku wakiwa kwenye mazingira mazuri, amini Manispaa itajivunia hiyo shule, tuombe Mwenyezi Mungu alifanikishe hilo”.alisema.
Katika mazungumzo yake nje ya kikao hicho Aesh anakusudia Shuke hiyo pia iwe na program maalumu za michezo ili kuwavutia wanafunzi wengi kusoma hapo.
Tayari Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya amependekeza eneo la hekari zaidi ya 20 la kujengwa shule hiyo katika moja ya kata kwenye Manispaa hiyo na mipango ikikamilika ya kupata ardhi husika itatangazwa rasmi.
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa