Sammy Kisika, mkabala na Udi wa Kipepeo wa Zumbe.
Moja ya changamoto kwa makundi mengi ya wanawake inatajwa kuwa kukosa umoja na mshikamano kwa mtu mmoja mmoja au kundi fulani, hali hii inatokana aidha kuwa ndoto za kufanikiwa kwa haraka au tamaa ya kila mtu kutaka kumzidi mwenzake katika mafanikio.
Hayo ni baadhi ya mambo tu katika safari ndefu ya maendeleo kwa kundi tajwa hapo juu ambalo mara kadhaa limekuwa likihubiri ushirikiano na kujinasibu kuwa hakuna maendeleo pasipo mtaja mwanamke.
Kuna ukweli mkubwa wa jambo hilo na hauwezi kulipinga, lakini wapo wanawake wanaojitambua na kuamini kuwa mafanikio hayo hayapatikani hivi hivi pasipo kamba ndefu ya kuwashika mkono wenzao wakaenda nao pamoja.
Mkoa wa Rukwa ni moja ya eneo ambalo inaaminika wanawake wengi wako nyuma kimaendeleo kutokana na sababu mbalimbali, yumkini ukifanya tafiti ndogo tu, utaambiwa yako mambo mengi yanayochangia hali hiyo ni kukosa mshikamano miongoni mwao na hata kiongozi wa aina yao kuwashika mkono waweze kuwa wamoja.
Oktoba 30, mwaka huu ilikuwa ni siku ya aina yake ambayo Wanawake wa mkoa wa Rukwa waliweza kushukuru kimoyomoyo na hata hadharani kuwa wanakubaliana na Mh.Rais Samia Suluhu Hassan kumhamishia moja ya askari wake shupavu, Tano Mwera kuwa Mkuu wa wilaya ya Kalambo akiunda safu na wenziwe wawili kuongoza wilaya za mkoa huo.
Kwanini Tano Mwera hapa? Baada ya kufika mkoani Rukwa akiwa katika wilaya ya Kalambo kwa haraka Mwanaharakati huyo wa maendeleo alianza kutafuta kapu ambalo litakusanya mawazo ya wanawake wa mkoa wa Rukwa na hata kuzibaini changamoto zao, ndipo alianza kuwaunganisha kuwa kitu kimoja.
Muunganiko huo ulizaa kitu kinaitwa “Wanawake Laki moja”, hii ikiwa ni Asasi ambayo inaunganisha wanawake wa mkoa wa Rukwa katika jukwaa moja kwa lengo kutafuta fursa mbalimbali ambazo zitamkwamua mwanamke.
Waweza kusema kuwa labda Tano Mwera ndiye kiongozi wa Jukwaa hili, lahasha yeye anasimama kama Mlezi tu ambaye wanawake hawa wa mkoa wa Rukwa kila mtu anamtaja na kukubali kwa ushauri wa Mlezi huyo ambaye anakuwa chini ya Mwenyekiti Goreth Matondwa na Katibu wake Kauye Ntemo wakuinda safu ndefu ya viongozi wa kundi hilo.
Uwapo wa Mlezi imara kwa Asasi ya Wanawake Laki moja mkoani Rukwa ni kumekuja wakati muafaka kwa wanawake hao ambao wanazalisha mazao mbalimbali, wanabuni vitu, wanasindika na mambo mengine mengi ambayo ukiwauliza wengi wao watakuambia hawafahamu masoko yako wapi.
Fursa hizo zote walizonazo wanawake wa Rukwa zilibainishwa Oktoba 30, wakati wa uzinduzi wa Asasi ya Wanawake Laki moja ambapo licha ya Tano Mwera kufanikisha ujio wa Wakufunzi mahiri waliowafundisha wanawake hao mada mbalimbali lakini pia alifanikiwa kuwaleta Mama Tunu Pinda (aliyekuwa Mgeni Rasmi), sanjari na Mbunge Mstaafu Vick Kamata ambao walichagia yale yaliyofanyika siku hiyo.
Achilia mbali maandamano ya wanawake hao yaliyozunguka mji mzima wakiwa wamevalia sare zao za gauni za vitenge vya njano na kuishia kwenye ukumbi wa Manispaa ya Sumbawanga wanawake hao pia walifundishwa masuala ya sheria mirathi, sheria za ndoa, sheria za ardhi na mbinu za kijasiriamali ambazo ni kikwazo kwa mwanamke wa mkoa wa Rukwa.
Tunalizungumzia jukwaa hilo kwa kulihusisha moja kwa moja na Mkuu wa wilaya Tano Mwera, hii inatokana na mahangaiko ya muda mrefu kwa wanawake hao ambao tunaamini hivi sasa wakiitumia Asasi ya Wanawake Laki moja wanaweza kupata darasa la mambo mengi kutoka ndani na nje ya mkoa.
Hapa Tano Mwera atumike kama mshika maono au ufunguo wa wanawake hao ambao watatafuta fursa zingine sehemu mbalimbali na kuzileta mkoani Rukwa, kisha tuone Mwanamke wa Rukwa anaendelea kubadilika na kuondokana na zile fikra ambazo siku ya uzinduzi zilitajwa kuwa ni pamoja kuoneana wivu, chuki na hata baadhi yao kutumia muda mwingi kukwamishana kwenye mambo yao, ihali Mlezi wao hakusudii kuona hayo yakiendelea kutokea.
Inawezekana kuwa wako akina Tano Mwera wengi hapa nchini lakini kwa Rukwa lazima tumpe sifa yake Mwanamama huyu kwa kile alichokifanya, huku tukiamini kuwa atakapotoa mguu wake kwenda sehemu nyingine serikali hata taasisi binafsi ataungwa mkono kwasababu anania ya dhati kumkomboa mwanamke wa mkoa wa Rukwa. Anapaswa kuungwa mkono.
Historia haidanganyi na yaliyomema yataonekana hata kwa maandishi siku zijazo, hivyo Asasi ya wanawake Laki moja inatakiwa kwenda kuwaibua wanawake maeneo ya mwambao mwa Ziwa Tanganyika na Rukwa kuwaaminisha kuwa wanaweza kufanya biashara ya kuuza samaki wao nje ya mkoa wa Rukwa pasipo kutegemea wanaume, aidha walio kwenye fursa zingine za kilimo nao pia waibuke na kusaka ngawira.
Mwenyekiti wa Asasi ya Wanawake Laki moja Goreth Matondwa anasema kwa kutegemea muongozo wa Mlezi wao wanataraji kuona mabadiliko makubwa kwa wanawake mkoani Rukwa na kipaumbele chao kwa sasa ni kuhakikisha ajenda ya maarifa ya ujasiriamali yanapandikizwa kichwani mwa wanawake wa mkoani humo.
Safari hii ni ndefu lakini mawazo ya mtu mmoja yakipewa nafasi na kufanyiwa kazi kwa kuungana na Wanawake wengine mkoani Rukwa wanayeza kuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi kwa wakazi wa mkoa wa Rukwa na daima wanachi wa mkoa huu watakumbuka kazi ya Mlezi wa Asasi hii ya “Wanawake Laki Moja.”
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa