Imeelezwa kuwa ni asilimia 34 pekee ya Wakazi wa mkoa wa Rukwa ndio wanaotumia vyoo bora hali ambayo inachangia uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa ya mlipuko ikiwapo kipindupindu na Polio kwa watoto.
Akizungumza katika maazimisho ya Siku ya Usafi wa Mazingira Dunia iliyofanyika katika Manispaa ya Sumbawanga Afisa Tawala Msaidizi Donald Nssoko aliyemwakilisha Mkuu wa mkoa wa Rukwa Makongoro Nyerere amesema takwimu hizo za uwepo wa vyoo bora ni chini ya muongozo wa kitaifa ambao unataka mkoa kuwa na angalau wastani wa asilimia 75.
Nssoko amesema takwimu hizo zinatokana na wananchi wengi wanaotumia vyoo licha ya kuwa sio vyoo bora ambavyo havikidhi vigezo vya miongozo ya sekta ya afya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Catherine Mashalla alisema program ya kufanya usafi katika Manispaa ni endelevu na kuongeza kuwa mkakati unapangwa ili kumwezesha kila mwananchi kufanya usafi kwenye eneo lake ilihali akiwaomba wananchi kuunga mkono mpango huo.
Naye Katibu Tawala wa wilaya ya Sumbawanga Gabriel Masinga alisema mpango uliopo unakwenda sanjari na kuanzisha mashindano ya usafi kwa wananchi na taasisi za kiserikali na binafsi ili kuchochea tabia ya wananchi kufanya usafi, huku akisikitishwa na vitendo vya baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakila miwa na kutupa ovyo maganda yake barabarani.
Masinga alisema tabia hiyo haileti sifa kwa wakazi wa Sumbawanga, kauli ambayo iliungwa mkono na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Justine Malisawa aliyewataka wakazi wa mji wa Sumbawanga kuhakikisha mji huo unang’ara kwa usafi kama ilivyo miji mingine inayosifika kwa usafi hapa nchini.
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa