Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya amewaagiza Watumishi wa sekta ya Afya ya halmashauri hiyo kuhakikisha wanasimamia miradi ya ujenzi wa iliyopo chini yao ili iweze kukamilika kwa ubora kama yalivyo malengo ya serikali.
Agizo la Mkurugenzi huyo limetolewaleo mara baada ya kukamilika kwa ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa vituo viwili vya afya vya Kata ya Molo na Matanga, zahanati ya Mponda na Nambogo, sanjari na ujenzi wa hospitali ya wilaya inayojengwa eneo la Isofu mjini Sumbawanga.
Mtalitinya alisema halmashauri hiyo imepata uzoefu mkubwa kwenye usimamizi wa miradi ya ujenzi wa madarasa ya fedha za Uviko-19, maarufu kwa jina la ‘Madarasa ya Mama Samia’ambayo ujenzi wake ulisimamiwa na Kikosi kazi cha halmashauri hiyo kikiongozwa na yeye mwenyewe, ambapo miradi hiyo ilikamilika kwa wakati na kuwa na majengo mazuri na bora, hivyo Idara ya Afya yapaswa kuiga mfano huo.
Alisema katika ujenzi wa majengo hayo ya afya yanapaswa kufuatilia kuanzia hatua ya msingi, kuta , paa na hata ukamilishaji wake ili kuondoa uwezekano wa kukutwa na dosari ambazo hazihitaji kuonekana kwenye halmashauri hiyo kwa sasa.
Aidha amemtaka Mganga Mkuu wa halmashauri hiyo kuhakikisha anateua timu yake ndani ya Idara hiyo (CHMT) ambao watagawanywa kwenye makundi kuweza kufuatilia kila kinachofanyika kwenye ,miradi ya afya kila uchwao badala ya kukaa ofisini na kusubiri taarifa kutoka kwa mafundi.
“Mganga Mkuu una kazi nyingi za kufanya na hutaweza kutembelea miradi yote kila siku, sasa yakupaswa kuunda timu ili ije moja kwa moja huku kushirikiana na Kamati za ujenzi ili kuweza kubaini na kurekebisha dosari yoyote inayoweza kujitokeza na kuitafutia ufumbuzi kwa haraka ili miradi yetu iendelee kuwa bora” alisema Mtalitinya.
Katika ziara hiyo ya Mkurugenzi aliyoambatana na timu yake yote ya Wataalamu wa halmashauri hiyo (CMT) alitoa nafasi kwa Wataalamu hao kuweza kutoa ushauri wao kwa kila mradi ili kuhakikisha inajengwa kwa ubora.
Manispaa ya Sumbawanga hivi sasa imepokea fedha kutoka serikalini na inajenga Kituo cha Afya cha Kata ya Molo kwenye kijiji cha Ulinji, kituo cha Afya cha Kata ya Matanga kwenye kijiji cha Kisumba na hospitali ya wilaya ya Manispaa hiyo kwenye eneo la Isofu lilipo kata ya Malangali kando ya barabara iendayo bandari ya Kasanga katika eneo hilo lililopo upande wa kulia katika eneo la makazi mapya.
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa