Anaandika Sammy Kisika.
Mkoa wa Rukwa umepitia kwenye historia kubwa ya mabadiliko ya huduma za kijamii na uchumi hadi hapa ulipo hivi sasa.
Moja ya changamoto kubwa ya mkoa huu ilikuwa ni suala la usafiri wa kufika makao makuu ya mkoa huo mjini Sumbawanga na hata wilaya zake. Wamiliki wengi wa vyombo vya usafiri walikuwa hawathubutu kuleta magari yao mkoa wa Rukwa wakihofia kuharibika kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara. Mathalani kutoka Mbeya kwenda Sumbawanga ambao ni umbali wa takribani kilometa 320 ulilazimika kutumia zaidi ya saa 10, kwa kusafiri barabara ya vumbi kwa kipande cha Tunduma –Sumbawanga.
Licha wa uwepo wa changamoto hizo za barabara alijitokeza Mzalendo huyo Hamoud Sumry kwa kushirikiana na nduguze wakaanzisha kampuni ya mabasi iitwayo Sumry High Class ambayo ilianza kwa kutoa huduma zao kutoka Sumbawanga kwenda mikoa ya Mbeya na Dar es salaam.
Kampuni hii ilifanya kazi ikipitia mazingira magumu ya barabara hizo kwa kuanza na basi moja lakini waliendelea hadi wakawa na mabasi mengi yaliyotapakaa sio tu mkoani Rukwa lakini pia kwenye mikoa mingine hapa nchini.
Kufanikiwa kwa kampuni hii ambako pia kulichagizwa na Mwanafamilia mwingine Salumu Sumry kulifanya mkoa wa Rukwa kuzidi kufahamika ndani na nje ya nchi ambako baadhi ya watu walikuwa hawaamini iwapo wamiliki wa mabasi hayo wanatokea mkoa wa Rukwa, hii ni baada ya kuwa na mabasi mengi ambayo yalikuwa yanatoka kwenye kituo kikuu cha mabasi Ubungo Jijini Dar es salaam wakishindana pia na Matajiri wengine wanaomiliki mabasi hapa nchini.
Lengo la Makala hii sio tu kusifia umahiri wa kampuni hii lakini namna walivyojitoa kuhakikisha Wanarukwa wanapata usafiri wa uhakika kwenda kwenye maeneo mbalimbali nchini, tofauti na baadhi ya matajiri ambao wako hivi sasa na mabasi yao ambao wamesubiri hadi barabara zijengwe kwa kiwango cha lami ndipo wamekuja kutoa huduma.
Miaka ya 1994 kampuni hii ilianza kwa kuwa na basi moja ambalo lilitoa huduma kutoka Sumbawanga kwenda mkoa wa Mbeya lakini taratibu ilizidi kunawiri na kuleta matumaini kwa Wanarukwa ambao sasa walikuwa na matumaini ya angalau kuzifikia safari zao tofauti na awali, mathalani wakazi wa maeneo ya mwambao mwa Ziwa Tanganyika iliwalazimu kutoka Kirando na kulala Namanyere, kisha Sumbawanga kwenda Mbeya na kupata basi la kwenda Dar es salaam.
Kampuni hii ilifanya mikakati ya uwekezaji kwa kuendelea kupanua wigo wa usafiri maeeneo ya vijijini pia ambako ilikuwa ngumu kwa Mwananrukwa kufika huko lakini Sumry High Class walijitahidi kuyafikia.
Pamoja na kuboreshwa kwa safari hizo ambazo wakati mwingine Kampuni hii ilijikuta kwenye lawama kubwa ya kujaza abiria kuliko kiasi, naweza nikasema kuwa ilitokana na wingi wa abiria ambao walihitaji kusafiri ihali mabasi yalikuwa macahache. Wangelifanyaje sasa, wakati wanahitaji kutoa huduma lakini pia kutengeneza faida?
Moja ya alama kubwa ya Kampuni hii iliyoongozwa na Hamoud Sumry na nduguze Salumu na Amour ni ajira nyingi walizozitoa kwa makundi ya vijana ndani na nje ya mkoa wa Rukwa ambako vijana hao walipata kazi ya Udereva, Kondakta, Wapiga debe, Wakatisha tiketi, wahudumu wa ofisi na wengineo wengi ambao walinufaika na familia zao kuweza kujikimu.
Kuyumba kwa Kampuni ya Sumry High Class kuliathiri watu wengi ambao walitegemea ajira kwenye kampuni hii, lakini bado baadhi ya waajiriwa wana muda wa zaidi ya miaka 20 ndani ya kampuni wakiwa wamepata ajira kwenye kampuni mwenza ya Sumry inayofahamika kwa jina la Morden Agrico Co’ Ltd ikijishughulisha na masuala ya Ukandarasi hapa nchini.
Wapo watu wamejenga, wamesomesha na kuendelea kuishi kutokana na kampuni hizi ambazo marehemu Hamoud na familia yake walizisimamia ni ungwana pia, hii ilitokana na ofisi zilizofunguliwa na Kampuni hii kwenye mikoa ya Rukwa, Mbeya, Iringa, Ruvuma, Mtwara, Kigoma, Tabora, Mwanza, Arusha, Dodoma na Dar es salaam na kwingineko.
Ukizungumza na familia hii akiwapo babao Mzee Mohamed Sumry atakuambia pia mafanikio yao hayakuwa rahisi bali nidhamu na matumizi ya fedha yalichangia kupata kile walichokihitaji kulingana na mazingira ya waliyoanzia kusaka riziki kwenye mji mdogo wa Laela ambao uko umbali wa takribani kilometa 100 kutoka mji wa Sumbawanga, ambako sio tu kwamba waliishi Laela lakini pia walipitia kufanya biashara za kuuza maharagwe, mahindi na bidhaa zinginezo za duka, lakini walithamini na kukilinda kipato chao kabla ya kuhamia kwenye biashara ya mabasi.
Hili ni jambo la kujifunza pia kwa kizazi cha sasa ambacho wana ndoto ya mafanikio kwa kupitia njia za mkato jambo ambalo sio rahisi katika uhalisia wa maisha yenyewe.
Wakati Hamoud akiwaza makubwa zaidi kupitia kampuni ya Morden Agrico Co’Ltd, Mwenyezi Mungu naye aliwaza ya kwake kwani Hamoud ambaye wiki mbili zilizopita alitoka Dar es salaam alikokuwa akiishi kwa muda mrefu kwenda Sumbawanga kwaajili ya kumsabahi babake Mzee Sumry na ndugu zake akina Salumu, alipata maradhi akiwa huko na kurudishwa Dar es salaam kwaajili ya matibabu.
Kwa mujibu wa Msemaji wa familia Salumu Shibibi anasema Hamoud aliugua na kulaza kwenye wodi ya wagonjwa mahututi kwenye hospitali ya Agakhan kwa muda wa siku mbili kabla ya kifo chake ambacho alisema kuwa kilisababishwa na homa Dengue.
Ama kweli vitu vizuri havidumu, lakini acha tuheshimu utukufu wa Mola aliyeamua kumwita Hamoud mbele ya haki, japokuwa Wanarukwa bado walikuwa wakimhitaji.
INNALLILAH WAINNAILLAH RAJUN.
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa