Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya amewasihi vijana wa Manispaa ya Sumbawanga kujitokeza kwa wingi katika shindano la kutafuta vipaji ili kuitumia fursa hiyo katika kuviibua na kuviendeleza vipaji vyao huku wakiitangaza Manispaa pamoja na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla.
Amesema kuwa kwa muda mrefu Mkoa wa Rukwa hasa wilaya ya Sumbawanga imekuwa na sifa ambayo wengi wakiisikia wanakuwa wanatishika hivyo shindano hili ni fursa ya kuonyesha mambo mazuri yanayopatikana ndani ya mji wa Sumbawanga na Mkoa. Ametoa wito kwa wananchi, vijana, pamoja na wazazi kujitokeza na kuwarusu vijana wao kuonyesha vipaji vyao kuvitumia na kuhakikisha wanajiimarisha siku zijazo kujipatia ajira.
“Idara ya maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na Afisa utamaduni tumeona tuwe na hili shindano ambalo litatumika kuibua vipaji lakini pia kuwaendeleza vijana ambao tunaaamini wakiendelezwa watatengeneza ajira, kwahiyo kipaji ni ajira, hivuyo niwasihi sana vijana wa Sumbawanga kutumia nafasi hii kuhakikisha kwamba wanaendeleza vipaji vyao,” Alisisitiza.
Kwa upande wake Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Sumbawanga, Kiheka Charles amesema kuwa manispaa ya Sumbawanga ina vipaji vingi na nia ya kuanzisha mashindano hayo ni kutoa muongozo kwa wasanii wenye vipaji mbalimbali kuweza kuyafikia malengo yao.
“Ofisi ya Mkurugenzi kupitia ofisi ya afisa utamaduni Manispaa ya Sumbawanga tuliamua kuandaa shindano hili lenye lengo la kuwasaidia vijana kuitangaza sanaa yao, kukuza vipaji vyao, na kuweza kuitumia sanaa kama chanzo cha ajira na kunufaika, hivyo basi tunaomba wasanii mbalimbali wenye vipaji wajitokeze kwa wingi kushiriki,”Alisema.
Halikadhalika, baadhi ya wasanii waliohudhuria kwenye mashindano hayo waliupongeza uongozi wa halmashauri kwa kuwathamini na kuwajali na kuomuomba aendelee kuwaibulia vitu vingine ambavyo vitakuwa ni fursa kwa vijana ili kuweza kuitangaza sumbawanga na Mkoa.
Mmoja wa washiriki wa mashindano hayo Switbert Filbert a.k.a Fire Music alisema “Tunamshukuru sana Mkurugenzi kwa kuanzisha shindano kama hili na tunamuomba kama kuna vingine anavifikiria avifanye kwasababu mkoa wa rukwa upo nyuma katika sanaa, michezo na mengine hivyo tunawaahidi watanzania, wanarukwa na Sumbawanga kuwa tutafanya vizuri.”
Aidha, mshiriki mwenzie wa mashindano hayo Daniel Benedicto a.k.a Dabeto alisema “Mashindano haya yakiendelea kwa Mkoa wetu wa Rukwa sana sana Sumbawanga tunaweza tukatoka sana kwasababu wasanii wengi hawapati muda wa kuonyesha vitu vyao wazi kama vile kupata fursa ya “ku-perform” mbele za watu, wengi tulikuwa tunahofu kwamba unaweza kuonyesha sehemu gani, wengi walikuwa wanjificha ndani, hii ni fursa ya kutengeneza mashabiki.”
Mashindano hayo ya “Sumbawanga Talent Search” yenye kauli mbiu “Kipaji ni Zawadi Thamini Sanaa Yako” yanasimamiwa na Afisa utamaduni ambaye pia ni msanii wa “Hip-Hop” aliyedhamiria kushirikiana na Mkurugenzi wa manispaa hiyo kuinua vipaji vya vijana wa Sumbawanga.
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa