Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini Aesh Hilaly ameiomba serikali kufikiria kuongeza kiasi cha fedha za ujenzi wa vyoo vya wanafunzi baada ya zile ambazo zimetolewa kwaajili ya ujenzi wa vyumba madarasa ili kukamilisha dozi kamili ya kazi hiyo kubwa iliyofanyika.
Aesh ambaye anaendelea kutembelea na kukagua miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye Manispaa ya Sumbawanga licha ya kumshukuru Rais Samia Suluhu kwa kutoa fedha hizo za ujenzi wa vyumba vya madarasa alisema kuwa katika ukaguzi wake amebaini kuwa shule nyingi zina changamoto ya vyoo ambavyo vinatokana na wingi wa wanafunzi.
Alisema kila shule aliyopita amekutana na maombi ya Walimu na wanafunzi ambao licha ya kushukuru kwa ujenzi wa madarasa hayo lakini kilio chao ni matundu ya vyoo.
Mbunge huyo wa Sumbawanga Mjini alisema ipo haja ya kuiomba serikali kulizingatia jambo hilo kutokana na hali hiyo ambayo inatishia usalama wa afya za wanafunzi na Walimu wao.
Akizungumzia ujenzi wa madarasa hayo Aesh alimshukuru Rais Samia kwa kubaini changamoto hiyo hususan katika kipindi hiki ambacho wanafunzi wa kidato cha Kwanza wanatarajia kujiunga na masomo yao mapema mwakani.
“Miaka mingine miezi kama hii tungelikuwa tumeshapokea maagizo kutoka Wizara ya TAMISEMI ambayo inatutaka wananchi na Watendaji wa halmashauri zetu kuhakikisha tunaongeza vyumba vya madarasa ili kuweza kuchukua wanafunzi wa kidato cha Kwanza kwenye shule zetu, lakini safari hii Mh.Rais ametusaidia sana kwa kutoa hizi fedha ambazo kila halmashauri inakimbizana kujenga madarasa yake”.alisema Aesh
Hatahivyo Aesh aliwaagiza Wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha wanajenga madarasa yenye viwango ili yaweze kudumu kwa miaka mingi huku wanafunzi wakiwa na uhakika wa masomo.
Aliwataka Wakuu wa shule hizo kujenga kwa kuzingatia bajeti na huku akiwataka kujiongeza zaidi ili fedha kidogo zitakazobaki zitumike kufanya vitu vingine vya maendeleo.
Manispaa ya Sumbawanga kwa mujibu wa Mkurugebzi wake Jacob Mtalitinya imepokea kiasi cha Shilingi Milioni 800.9, huku ikitakiwa kujenga vyumba vya madarasa 49, vine kati ya hivyo ni vya shule Shikizi.
Katika ziara hiyo Aesh ametoa mifuko Miamoja ya saruji kusaidi ujenzi wa vyoo kwenye Shukle ya Sekondari Sumbawanga ambacho ujenzi wake ulisimama kwa muda mrefu kutokana na mradi wake kuishiwa fedha, sanjari na choo cha wasichana kwenye Shule ya Sekondari Lukangao ambacho kilibomoka kwa muda mrefu, huku pia akisaidia mradi wa kupeleka maji kwenye Shule ya Sekondari Mhama ambayo ilikuwa haina maji.
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa