Imeendikwa na Sammy Kisika.
Jumla ya Majangili 481 waliokutwa na zana haramu wakizitumia kwaajili ya kuvua samaki kwenye Ziwa Rukwa wamekamatwa na kutaifishwa kwa mali zao zikiwapo nyavu haramu zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 170 ambazo zimeteketezwa kwa moto.
Kukamatwa kwa watu hao kunafuatia misako ndani Ziwa hilo kwa kipindi cha takribani mwaka mmoja ambapo Majangili hao wametiwa mikononi na Kikosi cha doria cha Pori la Akiba la Uwanda ambao wamefanikiwa pia kuwapiga faini la ya Shilingi Milioni 246.1 ambayo iliwahusisha wavuvi hao sanjari wafugaji waliokuwa wakichungia na kunywesha maji mifugo maeneo ya hifadhi ya Ziwa hilo.
Meneja wa Pori hilo la Akiba la Uwanda Orest Njau amesema kumekuwa na mikakati endelevu ya kudhibiti wavuvi kwenye Ziwa hilo na kuongeza kuwa katika kipindi hicho jumla ya Injini 25 za boti na maboti 19 yalikamatwa yakiwa yanavua kinyume cha taratibu ya maeneo ya hifadhi hiyo.
Njau alizitaja zana zingine zilizokamatwa ni pamoja na ngalawa 90, mitumbwi 72, baiskeli 31, mikokoteni miwili na matanki ya mafuta 17.
Alisema kikosi hicho kimekuwa kikifanya doria za ndani na nje ya Ziwa ili kukabiliana na vitendo hivyo vya uvuvi haramu ili kukabiliana na wavuvi wasiotii sheria kwenye kambi za Mahameni, Mchangani, Mashwiche iliyopo wilayani na mkoa wa Songwe.
Akizungumza katika zoezi la kuteketeza nyavu 141 za wavuvi hao, Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba alisema kuwa iko haja ya wananchi wa vijiji jirani kuwakumbusha wavuvi wanaovua kwenye Ziwa hilo historia ya muda mrefu ya Ziwa hilo.
Waryuba alisema kuwa iwapo vitendo hivyo haramu vikiendelea samaki ndani ya Ziwa hilo watatoweka na litabaki tupu huku wavuvi waliopo watandoka huku uchumi wa wakazi wa maeneo hayo ya Ziwa Rukwa ukizidi kuporomoka hivyo hawana budi kupinga vitendo vya uvuvi haramu.
Hatahivyo Mkuu huyo wa wilaya ameiomba serikali kupitia Wizara husika kupambana na kutoa maelekezo kwa viwanda vinavyozalisha nyavu hizo haramu kuacha kufanya hivyo badala ya mapambano na wavuvi pekee.
Ziwa Rukwa ni Ziwa linatoa kitoweo cha samaki aina ya Magege na Kambale wanaopendwa sana ndani na nchi jirani kama Jamhuri ya Kidemkokrasia ya Congo, achilia mbali wakazi wa Manispaa ya Sumbawanga ambao ni walaji wakubwa wa samaki hao.
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa