Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Thadeo Maganga amewataka wamiliki wa maghala yaliyopo katikati ya mji, wenye vibali na wasio na vibali, kusimamisha shughuli zao hadi kufikia mwezi wa kumi mwaka huu, na kufanya utaratibu wa kuhamia katika eneo la Kanondo, kata ya Ntendo, lililotengwa maalum kwaajili maghala na viwanda vidogo.
Maganga ambae pia ni afisa mipango miji wa manispaa hiyo amesema kuwa ofisi ya mkurugenzi wa manispaa ilitoa barua ya notisi kwa wamiliki wote ikiwataka kutekeleza agizo hilo na kubainisha kuwa katika kuhakikisha mji unakaa kwa mpangilio, manispaa imetenga eneo la Kanondo lililopo kata ya Ntendo maalumu kwaajili ya maghala na viwanda vidogo.
Kauli hiyo imetolewa baada ya diwani wa kata ya Majengo Mh. Dickson Mwanandenje kutaka kujua hatma ya utaratibu wa maghala yasiyo na vibali kuendelea kufanya shughuli zao katikati ya mji, swali ambalo aliliuliza katika kikao cha baraza ya madiwani hivi karibuni.
Katika ufafanuzi wake Maganga alisema kuwa kuna maghala nane yenye vibali ambayo yalijumuishwa kwenye michoro iliyopitishwa wakati mji unaanza ambayo yapo katikati ya mji katika kata za Mazwi na Jangwani na kuongeza kuwa kuna wamiliki wengine tisa walikodisha nyumba za watu na kuzigeuza kuwa maghala.
Kanondo ni eneo ambalo limetengwa kwa matumizi ya viwanda vidogo. Eneo hili lina ukubwa mita za mraba 773,039 lipo kando ya barabara ya kwenda Mpanda. Eneo litakalouzwa litakuwa na mita za mraba 553,422 sawa na ekari 136.7 lenye viwanja 153
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa