Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe ya Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Jacob Mtalitinya ameagiza kuundwa kwa Kamati za Lishe kuanzia ngazi za mitaa ili kuweza kunusuru watoto kutokana na hali ya udumavu.
Maagizo hayo yametolewa katika kikao cha Kamati ya Lishe ya Manispaa hiyo ikiwa ni utaratibu wa kawaida kwa wajumbe wa kamati hiyo kukutana kwa kila robo ya mwaka.
Mtalitinya amesema kuundwa kwa kamati hizo kutasaidia kampeni ya kuboresha lishe bora kwa watoto kwa kila familia kwani kila mzazi atapata fursha ya kukumbushwa aina ya chakula bora anachotakiwa kumlisha mtoto wake nyumbani.
Alisema katika kufanikishwa suala la lishe bora ni vyema wazazi washirikishwe katika kujadili namna ya kutengeneza utaratibu rafiki wa kutoa chakula kwa wanafunzi shuleni, kutokana na wanafunzi wengi kutumia muda mwingi wakiwa shuleni kuliko nyumbani.
“Utaratibu utakaotengenezwa uwe rafiki kwa wazazi na watajadili namna bora ya upatikanaji wa chakula na uwe wa hiari, ambapo ofisi ya Mkurugenzi inaweza kuufanyia kazi iwapo tu wazazi wenyewe watakuwa wameridhia pasipo vinyongo vya aina yoyote kwani tunafahamu kuwa suala la michango mashuleni linautaratibu wake ambao serikali imeelekeza na lazima ufuatwe.” Alisema Mtalitinya
Kamati hizo za Lishe katika Manispaa ya Sumbawanga zinatakiwa kuundwa kuanzia ngazi mtaa, vijiji, kata na hata halmashauri ambapo zinatakiwa kuundwa kabla ya Oktoba 30, mwaka huu ,kwa mujibu wa maagizo ya Mwenyekiti huyo.
Mkoa wa Rukwa ni moja ya mikoa inayotajwa kuwa watoto wenye udumavu kwa takribani asilimia 56 ya watoto wote.
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa