Zaidi ya vijana 100 ambao ni wahitimu wa vyuo katika ngazi ya Stashahada na Shahada wameshiriki kongamano la kujadili tatizo la ajira kwa wasomi hao na kutafuta namna ya kujikwamua kiuchumi.
Kongamano hilo ambalo liliandaliwa na Mkururugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya likiratibiwa na Idara ya Maendeleo ya Jamii katika halmashauri hiyo, limeshiriki Wananzuoni hao ambao wamehitimu katika kozi tofauti tofauti ikiwa ni pamoja na lengo la kubadilioshana uzoefu wa kitaaluma na mbinu mbalimbali za maisha.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya alisema kuwa halmashauri yake imeamua kuandaa kongamano baada ya kubaini kuwa kuna kundi kubwa la vijana ambao ni wahitimu wa vyuo wako mitaani na wakiendelea kulalamika kukosa ajira licha ya kuwa mkoa wa Rukwa una fursa nyingi za vijana kuweza kujiari wenyewe.
“Hivi sasa kuna wasomi wengi wanaohitimu vyuo vikuu, lakini bahati mbaya ni kuwa wengi wenu mnasubiri serikali iwape ajira jambao ambalo ni gumu kwa sasa, hivyo mnatakiwa kuzitumia changamoto hizo na kuzifanya kuwa fursa katika kupata ajira”.alisema.
Mkurugezi huyo aliwaambia wasomi hao kuwa mkoa wa Rukwa kuwa na ardhi ambayo kwa sehemu kubwa bado haijatumika kwa kilimo, lakini pia kuna fursa ya kujishughulisha ufugaji, uvuvi na hata usindikaji wa mazao mbalimbali.
Vijana hao pamoja na kufundishwa mbinu za uandishi wa maandiko mpango mradi katika mbinu za kujiari wenyewe, pia walipata fursa ya kujifunza kutoka kwa wataalamu na vijana wenzao waliothubutu kujikita kwenye miradi ya kilimo, ufugaji, mapishi na utengenezaji wa chaki ambao wengi wao wamewezeshwa na halmashauri hiyo kwa maarifa au mitaji yao.
Hatahivyo mara baada ya mafunzo hayo Mkurugenzi huyo wa Manispaa aliwataka vijana hao kuandika maandiko mengine ya miradi kupitia vikundi vyao au mtu mmoja mmoja ili wawezeshe kwa kupewa mikopo na halmashauri hiyo kwa kipindi cha mwezi Mei au Juni.
Hadi hivi sasa halmsahauri ya Manispaa ya Sumbawanga imekwishatoa mikopo zaidi ya Shilingi Milioni 170 kwaajili ya makundi ya vijana, wanawake na walemavu katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/19, ikiwa rekodi mpya kwa Manispaa hiyo kutoa mikopo kwa makundi hayo.
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa