KUTOKA JIKO LA NYAMA CHOMA KATUMBA-AZIMIO
Sammy Kisika, mkabala na Udi wa Kipepeo wa Zumbe.
“Ni ubunifu unaostahili kukumbukwa siku zote, lakini bahati mbaya sana binadamu tumekuwa tukitizama baadhi ya mambo pekee, ila katika hili kongele kwao Manispaa ya Sumbawanga”..kauli ya Mstaafu mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Palikuwa na mengi katika eneo hilo ambalo siku za nyuma palionekana kama vile pamepooza licha ya kuwa na majengo muhimu yanayohusu taasisi ya kilimo kinachozungumzwa kila uchwao mkoani Rukwa, halmashauri ikikitaja kuwa ni kituo cha kutolea mafunzo ya kilimo.
Haijalishi malengo yake lakini bado fursa hii hakiuchangamkiwa, hii inatokana na changamoto mbalimbali ambazo sio lengo langu kuzizungumzia kwa siku ya leo.
Hapa, nyama choma , pale ugali, huku kuku, pale samaki, muziki, vinywaji vya kila aina, iwe vya kisasa na hata vile vya asili, wanaotazama Farasi na kupanda nao pia walikuwapo,lakini uwanja ukajaa vyombo vya usafiri na watu wa rika tofauti waliokuja kushuhudia Mnada wa aina yake hapa Katumba.
Achilia mbali mbwembwe za ufunguzi zilizoshereheshwa na Mkuu wa mkoa wa Rukwa aliyechiwa jukwaa na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Andrew Zumba ambaye itifaki ilimwelekeza kumkaribisha Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba ambaye naye akamwachia Baba mwenye nyumba Mkuu wa mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ambaye awali watazamaji walidhani angelikuja na hotuba ndefu ya ufunguzi wa Nyama Choma Festival lakini yeye akaishia kuwakumbusha masuala ya fursa kisha Dansi likaendelea huku akigawa noti nyekundu nyekundu kwa wananchi waliocheza muziki.
Huyo ndiye Mkirikiti bhanaa ambaye ahakuhitaji kipaza sauti kuwaita watu kuwa waende wakamsikilize lakini ghafla walijaa wenyewe eneo la jukwaa wakishuhudia burudani.
Twaweza kusema kuwa hii ndiyo Manispaa tuliyokuwa tukiota siku zote, hongera kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya na Wakuu wako wa Idara kubuni mambo haya ambayo, wakazi wa mji wa Sumbawanga walikuwa wakijifungia ndani hawana sehemu ya kwenda wao na familia zao. Sasa kiwanja cha burudani kipo Ktumba Mnadani.
Eneo hili ni eneo zuri sana kwa mpango huu wa Nyama choma iwapo tu ukiwa ni endelevu, ukienda sanjari na uboreshaji wa mazingira yake ambapo kunaweza kujengwa mireji wa maji ya uhakika kwenye pande zote za Mnada huu ili kuondoa changamoto ya uwanja wa kutafuna nyama kujaa maji hususan nyakati za masika.
Sanjari na hiyo iwapo ningelipata simu ya Mkurugenzi wa Manispaa Mtalitinya basi ningelimwambia watu wanalikubali sana eneo hilo lakini ziruhusu kila Idara ibuni namna ya kuingiza pesa pale kwaajili mapato zaidi kwa halmashauri.
KITENGO CHA TEHAMA NA UTAMADUNI
Jengeni ukumbi mdogo wa Disko sanjari na mabanda Umiza ya watu kutazama mpira kwani mnada huu hufanyika wikiendi ambayo watu wengi hivi sasa ni wapenzi wa soka wanaweza kwenda Katumba lakini ikifika jioni wataondoka kukimbilia mjini kuwahi Runinga ili atazame Ligi ya Uingereza au Ligi Kuu Tanzania Bara.
Vibanda Umiza hivi visiwe bure tu, watazamaji watachangia angalau hata Shilingi Miatano, lakini pia yatengenezwe maeneo ya VIP kwa kiingilio cha Shilingi Efu moja au Elfu, watu wakae watazame soka huku wakishushia vinywaji vyao kando ya Nyama choma.
Lakini pia inawezekana nyuma ya eneo la Mnada upande wa Magharibi pakajengwa viwanja vya mpira kama wa Kikapu, Mikono na hata Bwawa la wastani la kuogelea (Swimming Pool) kwa watoto na watu wazima ili watu hao walipie na halmashauri itapata pesa.
MAENDELEO YA JAMII
Hapa panahitajika kuwa eneo la elimu endelevu kwa nyakati za mwanzo kabla ya mnada kuchanganya watu wawe wanapewa elimu ya Ujasiriamali labda twaweza sema kuanzia saa 4 hadi saa 6 kwa kila mtu kuchangia angalau Shilingi Elfu moja.
Pamoja na nyama hizo kuchomwa mnaweza kuanzisha mashindano ya nyama choma kila mwisho wa mwezi, hili lawezekana kwa kushirikiana na baadhi ya kampuni za vileo ambao wanaweza kudhamini mashindano hayo.
IDARA YA MIFUGO
Hakikisheni kando ya mnada huu kuwa na mnada mwingine wa mifugo na kila mfugaji anaweza lipia ushuru kwa mifugo ile tu inayouzwa lakini pia anaweza kutozwa Shilingi Elfu moja kwa kuingiza mifugo yake mnadani na hii itasaidia hata wafanya usafi eneo hilo wapate chochote badala ya kuitolea macho ofisi ya Mkurugenzi kuwalipa posho.
Haya ni yale yaliyotazamwa kwa leo na Meza ya Nyama Choma hapa Katumba lakini kwa kuamini weledi wa Wataalamu wa Manispaa mnaweza kubuni vitu vingine vingi katika eneo hilo ambalo baadhi ya walaji wanahitaji mwanga wa uhakika ambao utaangaza eneo hilo hata mpaka saa 6 usiku ili wapate burudani.
Ubunifu wa eneo hilo la Nyama choma Katumba liende sanjari na mabadiliko ya jina la Nyama Choma Festival badala yake liwe ni jina linaloakisi uendelevu wa jambo hili, lakini suala la hamasa kwa kujaribu kulinadi eneo lenyewe liwe ni endelevu kwa kila siku ili mtu apate shauku ya kwenda Katumba Mnadani kila Jumamosi apate utamu mpya sanjari na utalii wa vyakula, mifugo, watu na burudani.
Sanjari na hilo hata ile minada mingine kama ule wa Samaki Choma pale Mandela kila siku ya Jumanne na ule wa Siku ya Alhamisi pale Kamita nayo pia iwekewe mikakati kwani inaweza ikawa bora kuliko hata mnada wa Nyama Choma pale Loliondo-Kibaha au Nyama choma kule Mnadani-Dodoma.
Sumbawanga ya sasa ambayo inajiandaa kuwa Jiji huko mbeleni inahitaji vitu kama hivyo, kwani hata wale watani zangu waliokuwa wakidhani ujenzi wa Stendi ya Mabasi ya Katumba kuwa iko nje ya mji sasa wanakubali kuwa iko mjini kwani Jumamosi waliipita stendi wakaenda mbele zaidi kula Nyama choma.
Jiko hili la nyama choma limeshuhudia vijana wa Bajaji na Bodaboda wakipata ajira, Mama Ntilie wakitia noti nyekundu mifukoni mwao, Wauza vinywaji wakiuza vinywaji vyao hata juu ya Trekta, Wasanii wakipata motisha ya fedha kutoka hadhira iliyowazunguka wakitafuna nyama, lakini wengine wakifikiria kuwa walichelewa kutafuta viwanja vya kujenga nyumba huko Katumba. Wajasiriamali wakipata fursa ya kubadilishana mawazo kuhusu biashara zao na hata mahusiano mapya yenye uhalisia yakianzishwa.
Niwaage kidogo kwa leo, ngoja nikazungumze na Muuza mbuzi ambaye amesema ataniuzia kwa bei pooa kwaajili ya Jumamosi pale Katumba Mnadani.
Hongereni Manispaa ya Sumbawanga, sio lazima iwe hii leo lakini historia itaandikwa.
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa