Uongozi wa halmashauri za mkoa wa Rukwa umetakiwa kutumia Waandishi wa habari wa mkoa huo kwaajili ya kuhamasisha ukusanyaji wa mapato kwa halmashauri zao.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa mkoa wa Rukwa Zelote Stephen Zelote katika mkutano wa Wadau wa habari wa mkoa huo uliofanyika katika kilele cha Uhuru wa habari kwenye ukumbi wa Bomani mjini Sumbawanga.
Mkuu wa mkoa alisema kuwa halmashauri zimekuwa zikihangaika kuongeza mapato yake lakini zimekuwa zikikosa kiunganishi cha moja kwa moja kwa wananchi wake kutokana kukosa ushirikiano wa moja kwa moja.
Zelote alisema kuwa vyombo vya habari vikitumiwa vyema vinaweza kuwa msaada kwa kutoa elimu kwa wananchi ambao wataelewa umuhimu wa kulipa kodi na ushuru hivyo kuziwezesha halmashauri hizo kujiendesha kwa mapato yake.
Pia alizitaka halmashauri kutoweka urasimu wa utoaji wa taarifa mbalimbali ambazo zimekuwa zihitajika na Waandishi wa habari jambo ambalo limekuwa likiwavunja moyo wadau hao wa habari lakini pia hata halmashauri hizo zinakosa fursa ya kujitangaza ndani na nje ya mkoa.
“Unakuta Mwandishi anazunguka muda mrefu kutafuta habari kwenye ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri na anaambiwa nenda rudi siku na mwisho wa siku anakata tamaa”. Alisema Mkuu huyo wa mkoa.
Aidha katika mkutano huo wa wadau , uongozi wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoani Rukwa walimwomba Mkuu huyo wa mkoa kuwasaidia katika kufanikisha mchakato wao wa maombi ya viwanja kwaajili ya ujenzi wa ofisi ya klabu hiyo na makazi ya Waandishi hao wa habari.
Akijibu hoja hiyo Mkuu huyo wa mkoa alisema atahakikisha anafuatilia suala hilo na kumwagiza Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga kufuatilia suala hilo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga na majibu yake yapatikane ndani ya siku 30.
Mwisho
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa