Anaandika Sammy Kisika.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya amewatahadharisha wasimamizi wa miradi ambayo inajengwa kwa fedha zilizotolewa na Rais Samia Suluhu za ufadhili wa Uviko-19 kuhakikisha zinafanya kazi kulingana na malengo huku akiahidi kupambana na wote watakaokiuka maagizo ya Kamati ya ujenzi.
Manispaa hiyo imepokea kiasi cha Shilingi Milioni 980 kwaajili ya ujenzi wa madarasa 49 ya shule za Msingi na sekondari.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo ambayo ameitembelea na kutoa ushauri kwa Wasimamizi hao kwa muda wa siku tatu, Mtalitinya alisema kuwa anaamini Wakuu wa shule hizo watafuata yale waliyoelekezwa ili kuweza kukidhi vigezo vilivyotolewa na ofisi ya TAMISEMI kuhusu ujenzi huo.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa asingelipenda kuona halmashauri yake inaingia kwenye doa la kuwa chini ya kiwango kwa ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa hivyo ameamua kuweka mikakati kwa kuanza kutoa semina ya namna ya ujenzi wa miradi hiyo lakini pia yeye mwenyewe kupita kwenye maeneo yote ya ujenzi akiwa na Wataalamu ili kutoa ushauri wa kiufundi na mazingira.
Hatahivyo katika ukaguzi huo Mkurugenzi ametumia muda mwingi kukagua ubora wa madarasa hayo sanjari na maelekezo mengine ya matumizi ya kibajeti ili kuweza kuzitumia fedha hizo kwa usahihi.
“Haya majengo yajengwe vizuri na kwa ubora lakini pia yakamilike kwa wakati na jitihada za makusudi ziwekwe kuhakikisha ununuzi wa viti vya wanafunzi ili watakaoanza masomo kwa kidato cha Kwanza mwakani wasipate shida”.alisema Mtalitinya.
Aidha kwenye ukaguzi huo Mtalitinya ameoneka akitembea na Mkanda wa vipimo “Tape” kwaajili kuhakiki vipimo vyote vya ujenzi wa majengo hayo huku akikosoa pale ambapo vipimo na michoro imekiukwa au kukosewa.
Pamoja na ukaguzi huo Mkurugenzi huyo alisema utaratibu wa ujenzi wa miradi ya Uviko-19 umeonekana kuwa ni mzuri hivyo timu yake ya Wataalamu (CMT) imependekeza kuwa ni utaratibu wa kudumu ambao utatumiwa kwenye miradi ijayo ya halmashauri hiyo.
Katika utaribu huo mpya Wakuu wa Shule wanatakiwa kuwa kwenye eneo la mradi wakiwa na nyaraka zote za mradi, dodoso la maagizo waliyoyapata kwa Wataalamu na Mkurugenzi, sanjari na kupitia hesabu kila siku juu ya kile kilichoagizwa ili kuondoa uwezekano wa kufanya mambo mengine kinyume na mikataba ya miradi hiyo.
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa