Umoja wa madereva wa bodaboda katika manispaa ya Sumbawang, mkoani Rukwa wamehamasika kujitolea damu ili kukabiliana na upungufu wa upatikanaji wa damu katika vituo vya afya pamoja na hospitali ya rufaa ya Mkoa ili kuokoa maisha ya kina mama wajawazito na watoto wachanga.
Akiyasema hayo katika kuhamasisha madereva wenzie Mwenyekiti wa Bodaboda Mkoa wa Rukwa,Leonard Mirambo ameiomba serikali kuwa damu wanayotoa nao pia iwafae hasa pale wanapopata ajali na kuhitaji huduma hiyo katika vituo mbalimbali vya afya na kuomba kuthaminiwa kama wanavyothaminiwa makundi mengine katika jamii.
“Tunaishukuru serikali kwa jitihada zake za uboreshaji wa huduma za fya, sisi kama umoja wa madereva mkoa wa Rukwa hususan manispaa ya Sumbawanga tumehamasika kutoa damu ila kwa maana moja tu kwamba na sisi zitufae,” Alisema.
Kwa upande wake mganga mkuu wa manispaa ya Sumbawanga Dkt. Archie Heller amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo la kuchangia damu chini ya kauli mbiu ya mpango wa taifa wa damu salama “Jitolee kwaajili yaw engine, changia damu, kuzuia vifo vya mama wajawazito na watoto”.
“Mwaka 2017/2019 wajawazito 9 walipoteza maisha kwa kutokwa na damu nyingi kati ya vifo 33 vilivyotokea, ambayo ni sawa na 27% ya vifo kwa mama wajawazito wakati wa kujifungua, lakini licha ya damu hii wanayochangia kuokoa maisha ya wajawazito damu hii pia itatumika kuokoa maisha ya majeruhi wa ajali mbalimbali,” Dkt. Heller alisema
Nae mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Rukwa Dkt. John Lawi amesema kuwa hospitali nyingine za Mkoa wa Rukwa huomba damu kutoka katika hospitali ya mkoa na kufanya mahitaji hayo kuwa mengi zaidi na kusisitiza kuwa damu hiyo hutolewa bure na yeyote atakayedaiwa pesa, atoe taarifa itashughulikiwa.
“Hii damu zinazochangiwa sio zote zinazokidhi vigezo nyingine huishia kumwagwa na vipimo vya damu hii hufanywa hospitali ya rufaa ya Mbeya na wahitaji wengi wa damu ni kinamama wajawazito, watoto wachanga, ajali za barabarani hasa bodaboda lakini pia bajaji na magari na wagonjwa wa malaria wanaotoka ukanda wa ziwa Tanganyika na wa bonde la ziwa Rukwa,” Dkt, Lawi alisema.
Hali ya upatikanaji wa damu kwa sasa Manispaa ya Sumbawanga ni asilimia 46 sawa na chupa 240 kati ya chupa 520 zinazotakiwa kukusanywa kwa miezi 3, huku hospitali ya rufaa ya mkoa wa Rukwa ikitumia chupa 330 kwa miezi mitatu ambayo ni sawa na chupa 110 kwa mwezi.
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa