Anaandika Sammy Kisika.
Jeshi la Polisi mkoani Rukwa linawashikiliwa watu 42 kwa tuhuma mbalimbali, watatu kati yao wakituhumiwa kununua sanduku la risasi Elfu moja na Mianne zilizookotwa na wavuvi kwenye Ziwa Tanganyika, sanjari na askari watatu wa SUMA JKT ambao wanatuhumiwa kumpiga na kumsababishia kifo mkazi wa mji wa Namanyere wilayani Nkasi.
Katika tukio la kwanza Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa William Mwampaghale alisema kuwa watuhumiwa watatu wakazi wa kijiji cha Korongwe huko Nkasi wamekamatwa baada ya kununua sanduku moja lenye risasi ndani yake ambazo ni moja kati ya masanduku matatu yenye risasi 1493 zilizookotwa na wavuvi kwenye mapango ya yaliyopo kwenye mwambao mwa Ziwa Tanganyika kijijini hapo.
Kamanda Mwampaghale amesema risasi hizo ni za bunduki za kivita aina ya AK47 ambazo bado hazifahamika ni nani alizificha huko, lakini kitendo cha watu hao kujitokeza na kuzinunua risasi hizo kinyume cha sheria kinatia mashaka kuwa malengo yao yalikuwa ni yapi!
Pamoja na watu hao kukamatwa pia Polisi mkoani Rukwa linawashikilia watu wawili wakazi wa mjini Sumbawanga ambao nao wamekatwa wakiwa na risasi 14 za bunduki aina ya AK47 kwenye kitongoji cha Mazwi na Kashai.
Wakati hayo yakitokea Jeshi hilo pia linawashikilia askari watatu wa SUMA JKT ambao ni walinzi wa Chuo cha St.Bakitha cha mjini Namanyere na raia wengine wawili wakikabiliwa na tuhuma ya kumpiga hadi kumsababishia kifo mkazi wa eneo hilo wakimtuhumu kwa wizi
Sanjari na hilo pia Polisi mkoani Rukwa wamefanikiwa kumkamata mtuhumiwa anayetajwa kuwa ni mtuhumiwa sugu wa uvunjaji majumbani anayedaiwa kumwibia raia wa kigeni mwenye asili ya Kiamerika Kompyuta mpakato mbili sanjari na vifaa vingine vya kupikia chai aliponaswa navyo kwenye eneo la Kamwanda huko Kirando wilayani Nkasi.
Polisi mkoani Rukwa pia wamebaini kuibuka kwa wimbi la wizi wa pikipiki ambapo wezi hao wamekuwa na tabia ya kuzibadilisha injini na hata chesesi zake ili mradi tu kumchanganya mmiliki wake , ambapo katika msako wa mwezi mzima jumla ya watu 31 na pikipiki 21 wanashikiliwa kwa tuhuma ya vitendo hivyo.
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa