Ameandika Sammy Kisika.
Madiwani wanawake katika mikoa ya Rukwa na Katavi wametakiwa kushiriki kikamilifu kwenye upangaji wa bajeti za halmashauri zao huku wakiweka umakini katika utetezi wa makundi maalumu kwenye jamii zao.
Chachu ya Madiwani hao inatokana na mafunzo waliyoyapata ambayo yanaratibiwa na Mtandao wa Kijinsia TGNP ambapo imewakutanisha na kuwapa elimu juu ya njia bora ya kujadili bajeti katika mikoa hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo hayo aliwaambia Madiwani hao kuwa muda umefika wao kuonesha michango yao katika Mabaraza yao ya Madiwani badala ya kukaa kimya.
Mkirikiti alisema ipo haja ya Madiwani hao kuendelea kujengewa uwezo ili waweze kuhoji bajeti zinazopangwa kwenye miradi au huduma muhimu za afya, maji na elimu.
“Fedha nyingi zimekuwa zikitolewa kwenye miradi hiyo lakini hakuna anayehoji kuwa hapa kuna fedha hii ililetwa kwenye miradi ya afya au elimu, fungukeni sasa kwani huo ni muda wa kuitetea jamii ili huduma bora ziweze kupatikana”.alisema Mkirikiti
Alisema mchango wao katika jamii ni mkubwa hususan kipindi hiki ambapo Rais Samia Suluhu anaongoza, hivyo nao wanatakiwa kumuunga mkono kwa vitendo na kusimamia miradi inayofanyika kwenye maeneo yao.
Aidha Mkirikiti aliwapongeza TGNP kwa kuendesha mafunzo hayo ambayo anaamini kuwa maarifa wanayopata Madiwani hao yataleta mabadiliko kwa kuhoji mambo mengi yanayojadiliwa kwenye Mabaraza yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtandao wa Madiwani hao ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Lwiche katika Manispaa ya Sumbawanga Adolphina Konongo alisema anaamini kuwa hivi sasa wanauelewa wa kutosha kuhusu masuala ya bajeti tofauti na siku za nyuma ambapo walikuwa wakishiriki mabaraza yao na kukaa kimya muda mwingi.
“Nguvu yetu kubwa lazima tuielekeze kwenye miradi ya afya ambako zahanati zinajengwa na hakuna dawa, huku akinamama wakitembea umbali mrefu kufuata huduma hizo, hii sasa ifike mwisho maana tunapoteza wanawake na wazee wengi”.alisema Konongo.
Mratibu wa mafunzo hayo kutoka TGNP Clara Mcharo licha ya kufurahishwa na uelewa wa Madiwani hao aliwataka kujenga dhamira ya kweli katika kutetea masuala ya kiafya na huduma bora za kielimu kwa watoto kwenye maeneo yao.
“Utakuwa mzazi anakwenda jifungua zahanati anaambiwa aende na ndoo ili apewe kondo lake baada ya kujifungua, eti kwasababu zahanati au kituo cha afya hakina sehemu ya kuchomea uchafu, hii sio sawa, twendene tukapambane kwenye bajeti hayo mambo hayo yaishe”.alisema Clara.
Mtandao wa kijinsia wa TGNP licha kuwafundisha Madiwani hao namna ya kushiriki kwenye upangaji wa bajeti lakini wamefundishwa namna bora ya uongozi kwenye nafasi zao.
Sumbawanga Municipal Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 187, Sumbawanga
Simu ya Mezani: +255252802163
Simu ya Kiganjani: +255 735519681/ +255
Barua pepe: md@sumbawangamc.go.tz
HakiMiliki ©2017 Sumbawangamc . Haki Zote Zimehifadhiwa